Free Web Hosting by Netfirms
Web Hosting by Netfirms | Free Domain Names by Netfirms


Ukurasa wa mbele
Gazeti la injili
Nyimbo za Munishi
Soma barua Yahoo
Soma barua Hotmail
Tuma SMS duniani
Sema nami
Sikiliza waongo
Twende kanisani
Gazeti INJILI http://munishi.netfirms.com
E-mail: munishifaustin@yahoo.com
Or fmunishi@hotmail.com

Serikali Zahofia Nyimbo Za Injili

Nyimbo za Injili Afrika mashariki na kati zimepata kipigo kingine safari hii kutoka kwa serikali ambazo zinaziona kama tishio kwao. Mbali na matatizo yaliyokuwa yamezoeleka ya kunakili na kuuza nyimbo hizo bila kibali cha wasanii husika, sasa limekuja tatizo lingine kubwa ambalo linatishia kuzimaliza nyimbo za injili kabisa, hasa zile zinazoimbwa na wasanii binafsi.

Ni hivi majuzi tuliposhuhudia serikali ya Tanzania ikipiga marufuku kanda ya nyimbo za injili iliyoimbwa na msanii Faustin Munishi kwa kisingizio kwamba kanda hiyo ilikuwa imewagusa pabaya wanasiasa wa nchi hiyo.Pamoja na kwamba kanda hiyo haijafungiwa huko Kenya Uganda Rwanda na Burundi, lakini serikali za nchi hizo zimechukua hatua za tahadhari kuhakikisha kwamba wasanii wa Injili hawasikiki katika redio za mataifa hayo.

Kenya ambayo ilikuwa ikiongoza kwa kuwapatia wasanii wa nyimbo za injili nafasi katika redio na TV ya taifa KBC, sasa nyimbo hizo hazisikiki redioni kabisa. Sera za KBC kuhusu miziki ya dini zimebadilika ghafla jambo ambalo watafiti wa mambo wanaliona kama mpango madhubuti wa kumaliza nyimbo za injili kimya kimya.

Tanzania ambayo tangu mwanzo haijawahi kuwapa wasanii wa nyimbo za injili nafasi katika redio ya taifa, walilazimika kuzibiti njia zote zinazoingiza kanda za injili nchini mwao mpaka wakafanikiwa kuifanya kanda toleo la saba ya Munishi isiwafikie walengwa kwa kipindi chote cha uchaguzi. Hivi sasa kanda hiyo yenye nyimbo nzuri za kumtukuza Mungu inauzwa kwa maficho kama bangi au changaa. Pamoja na kwamba juhudi zao hazikufanikiwa kuifungia kanda hiyo kabisa, lakini wameonyesha kuwa kanda za injili ni tishio kwao.

Rwanda na Uganda wao wana mtazamo tofauti na wenzao wa Kenya na Tanzania. Kwao wanajali sana vyombo vya habari kuliko kanda za nyimbo. Kongo wakati wa Mobutu iliwahi kuzifungia nyimbo za wanamuziki wake lakini siyo wale wa kidini.

Serikali za Afrika zinajikuta mahali pagumu pa kutoweza kuchuja habari na ndio maana kwa makusudi zinachelewesha kila juhudi za kujaribu kurahisisha njia ya mawasiliano kwa watu wake.

Nikirudi Kenya ambapo vyombo vingi vya habari vimechipuka kama uyoga, bado kuna kazi kubwa mbele yao ili viweze kuonekana kuwa vinawasaidia wasanii. Vingi kama siyo vyote, havina tofauti na KBC kwa upande wa kuwapa wasanii wa injili nafasi ya kusikika.

Kameme redio ya kibinafsi inayotumia zaidi lugha ya kikuyu imefanya tofauti na redio nyingine kwa kuwapa kipaumbele wasanii wa Kenya na hasa wakikuyu, lakini hata hivyo haikuwasaidia sana wasanii hao kwani watu wameacha kununua nyimbo za wasanii hao na kutegemea kuzisikia kutoka kameme.

Nasema nini? Nataka wapewe nafasi ya kusikika na isipite kiasi. Muhimu zaidi ni kujua serikali zinachangia kuyasababisha matatizo yanawakabili wasanii sasa hivi. Ikiwa serikali inaweza kuwatumia maofisa wa usalama wa taifa, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja Polisi kuhakikisha kuwa kanda ya Munishi haionekani popote Tanzania, kwa nini wasiweze kuzuia wale wanaonakili kanda hizo bila kibali? Wanaweza kuwazuia lakini hawataki. Kwa nini? Wanajua wao.Watafiti wanaona kuwa moja ya sababu ni kuhakikisha wasanii hawainuki kiuchumi ili wawe rahisi kununuliwa na serikali kuimba sera zao.

Wasanii wenyewe ndio wanaoweza kutatua matatizo yanayowakabili na siyo serikali. Paka hawezi kumsaidia panya kujenga nyumba imara, na sababu wote tunaijua. Vivyo hivyo serikali haiwezi kuwasaidia wasanii ambao kwao ni tishio.

Serikali za Uganda na Tanzania zinayajua makampuni haramu ya kimataifa yanayofanya kazi nchini mwao ya kunakili na kuuza kazi za wasanii bila kibali, cha ajabu haziyachukulii makampuni hayo hatua zozote za kisheria. Inasemekana kuwa baadhi ya wakuu wa serikali wana hisa katika makampuni hayo.

Ndiyo maana wasanii wa dunia nzima wanapolia kuwa kazi zao zinaibiwa Uganda na Tanzania hakuna chochote kinachofanywa na serikali hizo. Kenya kuacha wezi binafsi wanaosambaza nakili zilizotoka Uganda na Tanzania hakuna kiwanda cha maharamia kilichopewa leseni na serikali kuendesha biashara haramu ya kuwahujumu wasanii kama ilivyo Uganda na Tanzania.

Siyo kwamba Kenya ni wazuri kuliko wenzao lakini wao wanaifanya tofauti kidogo. Badala ya kuwamaliza kabisa wasanii iliowajenga, serikali ya Kenya inawatafuta wale wanaokubali kununuliwa na ikishawanunua inawatumia kwa faida ya serikali. Na wale wanaokataa wanazimwa kimya kimya au ikibidi hadharani.

Hata siasa za Kenya ni tofauti kabisa na Tanzania.Badala ya kutumia risasi kuwaua watu zaidi ya hamsini huko Zanzibar kwa kisingizio cha kuandamana bila kibali cha serikali, Kenya wangehesabu gharama ya risasi pamoja na madawa kwa majeruhi waone ni milioni tisa.Halafu wahesabu chakula cha mahabusu wa tukio waone ni milioni tano.Kisha wahesabu hongo kwenye media kuutetea uongo waone ni milioni kumi. Jumla zote zije Kshs.milioni 24 kisha wamwendee Shariff Hamad wamwambie tunaona badala ya kuuwa watu wewe chukua milioni 200 ya tanzania ambayo ni milioni 20 ya Kenya na waambie watu CUF na CCM zinaungana kuwa kitu kimoja. Halafu kazi iwe ni kwa Shariff Hamad aamue kusuka au kunyoa. Mkapa aje kwa Profesa wa siasa Moi amfundisha alimpa nini Odinga mpaka akaimba nyayo.

Bado msimamo wangu kwa wanasiasa ni huu. Kwamba

Wanasiasa ni wezi wanaotaka walindwe na sheria, ileile waliyoivunja wakiingia madarakani. Waliingia isivyo halali, wanataka watolewe kihalali. Walipitia dirishani, wanataka kutokea mlangoni. Hawaoni haya kuitumia sheria wasiyoitii iwasaidie kuwaweka kizuizini wote wanaowataka watoke madarakani kama walivyoingia. Wanasahau sheria ni Msumeno unaokata kuwili. Wanataka sheria iwazuie wengine wasiibe, lakini waibe wao. Mwisho wao umefika, wametuibia vya kutosha. Sasa tunataka mapinduzi ya kuwatoa wezi kama walivyoingia.

Ikiwa waliingilia dirishani wakiwa wembamba, watatokea hapo hapo baada ya kunenepa kwa mali za wizi. Wananchi tumeanza mapambano ambayo hayatanyamazishwa na mtutu wa bunduki, bali haki kwa kila binadamu itakapotendeka, ndipo vita yetu itakoma. Wanatumia sheria walizozitunga wenyewe wakashindwa kuzitii, sisi tutatumia sheria za Mungu atupaye uwezo wa kuzitii.

Kinyume na sheria za wanadamu zilizo na upungufu, sheria za Mungu ni kamili. Yeye hana upendeleo kwa mtu awaye yote. Mungu alisema tuzitii mamlaka, lakini zile tu zinazotoka kwake. Torati na manabii wote walikuwa kinyume na mamlaka dhalimu, sioni kwa nini sisi tunaohubiri Injili ya Yesu Mwokozi tukubaliane na udhalimu huu.

Yesu mwenyewe aliwaita wanasiasa mbweha sioni sababu ya sisi kuwaita waheshimiwa. Wanaheshimiwa kwa nini? Eti walianzisha taifa? Mungu ndio mwanzo wa kila kitu. Eti walitutoa katika minyororo ya wakoloni? Ni nini ikiwa walipotutoa minyororo walitufunga ya kwao? Wanasema walitujengea vituo vya afya? Mbona havina dawa? na zile zilizoko mwananchi hawezi kumudu gharama zake? Mbaya zaidi wao wenyewe hawatibiwi huko.

Lakini Mungu hana upendeleo, kwani anahakikisha kuwa wanasiasa wanapokwenda ngambo wakiwa moto kutafuta huduma nzuri za kiafya, wanarudi wakiwa baridi pamoja na juhudi zote za kujaribu kuyaokoa maisha yao. Na wananchi walioachwa na zahanati ambazo hazina dawa, Mungu anahakikisha kuwa chochote watakachokitumia kama dawa kinawatibu na wanapona kabisa, ili Mungu abaki kuwa Mungu, na wanasiasa wabaki kuwa wanadamu waongo.

Kuna uvumi kuwa siasa duniani zinaendeshwa na makundi ya watu waovu ambao hutegemea mapato haramu kutoka katika biashara ya madawa ya kulevya, pamoja na magendo ya kila aina. Ni makundi hayo ndiyo yanayoamua nani awe kiongozi wapi ili mradi maslahi yao haramu yalindwe. Wanatumia mabilioni ya pesa kushinikiza chaguzi zote duniani. Wanaoshinda uchaguzi siyo wale wanaopendwa na wananchi wa nchi husika, bali ni wale ambao sera zao zinalinda maslahi ya majambazi hao wa kimataifa.

CCM chama kinachotawala Tanzania kwa sasa, siyo kwamba kinapendwa na umma wa Watanzania, bali ni chama cha majambazi wa Tanzania kilichofadhiliwa na wenzao wa kimataifa ili kulinda maslahi yao. Ndio maana tunasema kwa ujasiri kuwa siasa ni uongo na dunia haifai kuongozwa kisiasa. Dunia ni ya Mungu, na inafaa kuongozwa kidini. Na huu ndio wakati unaofaa kufanya mageuzi hayo. Wanasiasa pamoja na waandishi wa habari wanaojiita Third Estate, wameshirikiana kuifikisha dunia mahali ilipo. Sasa ni wakati wetu watumishi wa Mungu au kama tunavyojulikana First Estate, kuiokoa dunia isiangamie.

Ameandika Munishi Faustin

 

 
| http://munishi.netfirms.com |
 
<<Back  |  Home |  Gazeti La Injili | Injili2 | Nyimbo Za Munishi | Next >>